Idara ya Watoto na Shule ya Jumapili

Image

Idara ya Watoto na Shule ya Jumapili, ni idara inayolenga katika kuwalea watoto katika njia ya kumjua Bwana wetu Yesu Kristo toka utoto wao, na kuwatayarisha kuingia katika mafundisho ya Kipa Imara. Kwa sasa idara hii inaongozwa na Ndugu Donald Mwakatobe ambaye ndiye Mwalimu Kiongozi wa Idara ya Watoto na Shule ya Jumapili, akisaidiwa na walimu wenzake.

Kanisa limeweka shabaha ya Idara ya watoto na Shule ya Jumapili kuwa ni kama  ifuatavyo:

  • Kuwalea watoto katika hali ya kumjua na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo, tangu utoto wao na kuwatayarisha kuingia katika mafundisho ya Kipa-imara.
  • Kuwaelimisha namna ya kumtumikia Mungu kwa kutumia vipawa vyao vya kuimba, kuchora, michezo na ufundi mwingine.
  • Kuwalea katika mazingira mema ili waweze kuwa raia na viongozi wema wa baadaye.

Watoto hukutana kila siku ya Jumapili asubuhi kwa ajili ya mafundisho ya elimu ya Biblia na pia kumsifu Bwana. Watoto hugawanywa katika makundi kutegemeana na umri wao. Hivyo hata mafundisho yao pia hutegemea umri wao. Kila kikundi hukaa peke yake na mwishoni watoto wote hukusanywa pamoja kwa ajili ya kutoa sadaka.

Watoto wameunda kwaya yao ambayo inaitwa Young Wisdom. Kikundi hiki cha uimbaji ambacho hujumuisha watoto wa rika zote, mpaka sasa kimeisharekodi nyimbo zake ambazo hupatikana kwenye mfumo wa Audio na DVD. Watoto hukutana siku ya Jumamosi kwa ajili ya kujifunza nyimbo. Mbali na shughuli ya kujifunza neno la Mungu na uimbaji, shule ya Jumapili hujihusisha na shughuli nyingine kama vile kuwatembelea watoto waishio kwenye mazingira magumu, n.k.

Mwalimu  Kiongozi  wa  idara  ya  Watoto  na  Shule  ya Jumapili  huangalia mahitaji ya watoto kiroho, kimwili na kutafuta njia za kuwasaidia, hufanya Uinjilisti kwa watoto wasio wakristo ili wajiunge na wenzao katika kumjua Kristo, huangalia shida za walimu na kuwasaidia inapowezekana, hutembelea watoto katika mitaa yao, pamoja na kuwashauri   wazazi   ili   wawahimize   watoto   kuhudhuria shule ya Jumapili.  

Baba Mchungaji Gentleman Mwansile ni Mlezi wa Idara hii.